MMONYOKO WA MAADILI MAENEO YA KAZI

      1 Comment on MMONYOKO WA MAADILI MAENEO YA KAZI

Ofisi nyingi zimekuwa zikinyooshewa vidole kwa sababu ya kuwa na watu wasio waadilifu. Miaka ya hivi karibuni vitendo vya mmonyoko wa maadili vimekuwa vikiripotiwa kwa wingi kuliko miaka iliyopita. Maeneo ambayo yamekuwa yakitajwa mara kwa mara ni rushwa, wizi, ubadhilifu, udanganyifu, unyanyasaji na ubaguzi. Imefika hatua watu wamekuwa wakihusianisha rushwa na upatikanaji wa kazi, kupanda vyeo na kupata manufaa mbali mbali maeneo ya kazi.

Japo serikali na vyombo vya ulizi na usalama vimekuwa vikipigania kudhibiti vitendo hivi lakini bado vimeendelea kushamiri.

CHANZO

Mijadala ya nini ni chanzo cha mmonyoko wa maadili makazini imekuwa ikifanywa na watu huku majibu yakikinzana kwa sababu mbali mbali. Mathalani, suala la ruswa watu wamekuwa wakilihusisha na ujira mdogo lakini sababu hii huonekana aidha ina mchango mdogo kwenye tatizo au ni hulka tu ya mtu kwani hata wale wanaopokea ujira unao onekana ni mkubwa kupita kawaida bado wameendelea kushiriki katika vitendo vya rushwa.

Suala jingine linaloweza kuwa chanzo cha matatizo yahusianayo na maadili kazini ni mmomonyoko wa maadili katika jamii kwa ujumla. Watu tunaokutana nao katika maofisi ndiyo hao hao tunaokutana nao mtaani; ni sawa na kusema kazi au ofisi ni sehemu ya jamii. Mmomonyoko wa maadili kimekuwa kikionekana kama ni kitu cha kawaida katika jamii hivyo kupelekea kuhalalisha au kuona ni kitu cha kawaida hata katika maeneo ya kazi. Ukigoma kutoa  au kupokea rushwa kwa sababu za kimaadili unaonekana ni mshamba uliyepitwa na wakati.

Dhana ya kwenda na wakati ni suala la kutazamwa katika mmomonyoko wa maadili. Taasisi nyingi binafsi na za serikali zina sera na miongozo yenye lengo la kudhibiti mmomonyoko wa maadili lakini zimekuwa zikionekana ni haziendani na wakati. Suala la mavazi ni moja ya mambo yanayotazamwa sana au kuwekewa miongozo lakini bado imekuwa ikionekana ni usubufu usio wa lazima.

Ushawishi wa makundi pia ni moja ya vyanzo vikuu vya kujiingiza katika vitendo vinavyo ashiria mmomonyoko wa maadili. Watu wengi hufanya kitu kwa sababu wengine wanafanya. Kuiga mambo kumefanya kansa ya mmomonyoko wa maadili kuzidi kusambaa kwa kasi. Ni vigumu sana kwa watu wengi kuacha kupokea rushwa kama mabosi wao wanaendekeza vitendo hivyo.

Mbaya zaidi rushwa imeendelea kukua na kubadili hadi aina ya vitu vinavyo husishwa katika mchakato wa rushwa na kufikia hadi kiwango cha rushwa ya ngono ambayo huwatesa wengi kisaikolojia na wakati mwingine kusababisha  hata matatizo ya afya ya mwili na akili.

 

MADHARA

Mmomonyoko wa maadili umeendelea kuwaathiri watu, taasisi na nchi kwa ujumla. Watu wamekuwa wakipoteza haki zao kisa wameshindwa kutoa chochote na wengine wapokea kile wasichostahili eti kwa sababu tu wana uwezo na utayari wa kushiriki vitendo vya rushwa.

Watumishi wengi ambao wamekuwa wakijihusisha na masuala haya wamekuwa wakijutia maamuzi yao pindi wanapo bainika. Wapo waliopoteza kazi zao na wengine kuishia kwenye mikono ya vyombo vya ulinzi na usalama kwa sababu tu walishiriki vitendo hivi.

Taasisi na nchi imekuwa ikiingia hasara kutokana na baadhi ya watu kuchukua maamuzi yasio na tija kwa taasisi zao na taifa kwa sababu tu ya kushiriki rushwa iliyosababisha upendeleo. Watu wasio na uwezo wanapewa ajira, tenda na vyeo ambavyo hawakustaili na hivyo  hushindwa kuvimudu na kuharibu kazi za taasisi.

Taswira ya baadhi ya taasisi zimekuwa zikiharibiwa na matendo haya na kuharibu sifa njema zilizojengwa kwa muda mrefu sana. Hii imefanya taasisi hizo kushindwa kuaminiwa au kukubalika na jamii inayozizunguka.

USHAURI

Ni vyema kwa watumishi katika sekta binafsi na sekta ya umma kutambua majukumu yao na kuweka maslahi ya taasisi mbele na siyo maslahi yao binafsi. Kumnyanyasa au kumuonea mtu kwa sababu ya chuki au sababu yoyote ile ni kukosa uadilifu na kushindwa kutimiza majuku yako ya msingi.

Viongozi katika taasisi zote licha ya kutakiwa kusimamia  sheria, miongozo na taratibu katika kulinda maadili wanatakiwa pia kuwa mfano kwa watu wanaowaongoza. Kiongozi mwizi asitarajie kuwa na wafuasi wenye maadili mema. Mara nyingi wafuasi hawafuati maneno ya kiongozi bali matendo na endapo yatakinzana na maneno yake ni vigumu sana kwa wao kuheshimu miongozo ya kiutumishi.

Taasisi pia zinatakiwa kuhakikisha zinakuwa karibu na wafanyakazi kupitia viongozi wa taasisi au idara husika ili kujua shida na mahitaji yao. Kudhani kuwa kila kitu kiko sawa bila udadisi ni kutengeneza mazingira ya watu kujichukulia maamuzi wanayoona yanafaa na kudhani pia pengine hawapendwi na taasisi zao.

Watu uwa na taarifa nyingi ambazo hawawezi zisema mpaka waulizwe. Inawezekana haupokei wala hautoi rushwa lakini ukimya wako na kutokujali kumesababisha wengine wafanye hivyo. Inawezekana unaona unavyo vaa ni kawaida lakini bila kujua ukawa unawahamasisha wengine wavae nguo zisizo za maadili.

Pia ni vyema kujifunza kuridhika. Kuna msemo unaosema ‘pesa haijawahi kutosha’; hii inamaanisha hata ukishinda bahati nasibu leo ambayo haukuitarajia bado utaipangia bajeti na utaona haitoshi. Mishahara nayo haijawahi kutosha pia hivyo ni vyema kujifunza kuridhka na kujiepusha na vitendo vya rushwa vinavyoweza kugharimu kazi yako na muda wako bila sababu za msingi.

Mwisho, maadili sehemu yoyote yanaanza na mtu mmoja kwanza. Kila mtu akizingatia maadili mema suala la mmomonyoko wa maadili sehemu yoyote halitakuwa na nafasi. Usifanye upumbavu eti kwa sababu fulani kafanya.  Upumbavu hata ukifanywa na watu wote bado hauwezi kubadilika kuwa hekima.

Facebook Comments

1 thought on “MMONYOKO WA MAADILI MAENEO YA KAZI

  1. Pingback: MMONYOKO WA MAADILI MAENEO YA KAZI – Kelvin Mwita

Leave a Reply

Your email address will not be published.