UMUHIMU WA DHANA YA USHIRIKISHAJI KWENYE MAAMUZI YA TAASISI

Taasisi yoyote hustawi vyema kama imejengwa katika misingi imara ya umoja na ushirikiano katika ngazi zote.  Lengo kuu la kuunda taasisi ya iana yoyote ni kuunganisha nguvu ya zaidi ya mtu mmoja ili kufikia malengo ambayo mtu mmoja asingeweza kuyafikia. Kama lengo fulani linaweza kufikiwa kwa ufanisi na mtu mmoja basi hakuna haja ya kuunganisha nguvu na kuunda kikundi, timu au taasisi.

Katika mazingira ya kawaida watumishi au wafanyakazi ushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha  wanatumia vyema rasilimali zilizopo ili kufanikisha malengo haya. Kwa bahati mbaya na wakati mwingine kwa makusudi baadhi ya viongozi au hata watumishi wa kawaida udhani kuwa hakuna umuhimu wa ushirikishaji katika maamuzi ya kitaasisi. Maamuzi haya yanaweza kuwa katika ngazi ya chini kabisa na wakati mwingine ngazi ya juu ya maamuzi. Kukwepa kuwashirikisha wadau muhimu katika mustakabali wa taasisi yoyote ni kuamua kuigawa na pengine kuiua taasisi taratibu.

NAMNA YA KUFANYA USHIRIKISHAJI

Kufanya maamuzi si tukio bali ni mchakato. Na mtu anapofanya maamuzi ni dhahiri ana mbadala wa machaguo, bila mbadala hatuwezi sema kuwa mtu anafanya maamuzi na ndiyo maana watu usema ‘hata kutokuamua ni kuamua pia’ kwa sababu umechagua kutokufanya. Kwa sababu wakati wa kuanya maamuzi kunakuwa na mbadala wa machaguo ukweli ni kwamba chagua bora kwako linaweza lisiwe bora kwa mtu mwingine nan i vyema kulifahamu hilo kwanza.

Katika kufanya maamuzi  kuna mambo kadhaa ya kuzingatia; kwanza, uharaka wa maamuzi na uzito wa maamuzi yenyewe. Matumizi ya vikao na mijadala ya ana kwa ana kati ya mtu mmoja na mwingine hutumika mara kwa mara katika kushirikisha wengine katika kutoa maamuzi.

Njia ya mikutano na vikao mara nyingi ni bora zaidi kwa sababu ni njia ya uwazi zaidi. Lakini changamoto ya njia hii ni matumizi muda mwingi kufikia maamuzi na hivyo kufanya mchakato kuwa mrefu zaidi. Kwa maamuzi yenye kuihitaji uharaka njia hii si nzuri zaidi kuitumia

Njia nyingine ni ya uwakilishi, si mara zote fursa ya kukutana na kila mtu au watu wote hupatikana hivyo katika mazingira haya njia ya uwakilishi ni bora zaidi. Wakati mwingine ni vyema kutafuta watu wa chache watakao wawakilisha wengine ili kufikia maamuzi fulani. Kwa masuala yenye uharaka njia hii ni bora zaidi kuitumia kwani uokoa muda.

Changamoto ya matumizi ya njia hii ni pale watu wanapohisi hawakuwakilisha ipasavyo au kikundi fulani kuhisi kuwa uwakilishi wao haukuwepo kwenye maamuzi husika. Mathalani, wakuu wa idara zote wameitwa katika kufanya maamuzi lakini kuna idara ambayo haikupata mwakilishi. Suala hili linaweza kuharibu dhana nzima ya ushirikishaji.

Katika dhana ya ushirikishaji wakati mwingine kiongozi anaweza kutumia fursa hii kuwashawishi watumishi au wafuasi wake juu ya kile anachokiamini au juu ya maamuzi anayotaka kuyachukua. Ukweli ni kwamba mara nyingi viongozi wanapokuja kuomba ushauri tayari nafsini mwao wanakuwa wameshafanya maamuzi hivyo kinachoanyika ni kutafuta baraka za maamuzi yao. Kabla ya kutekeleza maamuzi yako tafuta muda wa kushawishi kwa nini unadhani wazo lako ni bora. Kufanya hivi ni bora zaidi kuliko kufanya maamuzi kimya kimya.

MADHARA YA KUTO KUSHIRIKISHA

Baadhi ya watu hudhani kuwa hakuna shida yoyote pale mtu mmoja anapoamua kutumia mamlaka yake kutoa maamuzi yanayo athiri watu wengi. Katika kanuni za kiuongozi hili ni moja ya makosa makubwa sana. Kitendo hiki uathiri ushirikiano na kuigawa taasisi.

Wakati mwingine watumishi kwa makusudi kabisa uamua kupunguza ufanisi ili maamuzi yaliyotolewa na kiongozi au bosi wao yasilete matokeo yenye tija kwa lengo la kuthibitisha kuwa peke yake hataweza kufanikiwa.

Watu pia hutoa tafsiri kuwa kongozi au bosi wao ni dikteta. Utoaji wa maamuzi hata kama ni madogo unaweza kuwa na athari kubwa sana kwenye taswira ya kiongozi kwa wafuasi wake. Usikubali kuharibu sifa yako njema kisa tu umeshindwa kuwauliza watu “mnaonaje wazo hili”.

KWA NINI WATU WASHIRIKISHWE

Kwanza,  utofuati tulionao sisi binadamu ni moja ya sababu kubwa kwa nini wengine washirikishwe katika maamuzi ya kitaasisi na hata yale yasiyo ya kitaasisi. Kila mtu ana vitu anavyofahamu ambavyo mtu mwingine havifahamu kabisa. Wazo unaloliona ni bora pengine utapowashirikisha wengine wanaweza kukupa taarifa ambazo zitakufanya uone kwamba endapo ungetumia wzo hilo kufanya maamuzi yako yangekuwa maamuzi ya kijuha na si ya busara kama udhaniavyo. Kwa kifupi, usimdharau mtu yoyote yule unayemjua na hata yule usiyemjua.

Ushirikishwaji unaongeza hamasa ya kazi; watu uhamasika zaidi kufanya kitu wanachoamini ni matokeo ya maamuzi yao. Mara nyingi watu ukipa muda na umakini kile kilicho chao kuliko kile ambacho si chao hivyo endapo watashirikishwa mapema inawaongezea hamasa ya kushiriki vyema katika utekelezaji.

Kitu kingine ambacho ni cha msingi sana ni uwajibikaji wa pamoja. Si kila maamuzi uwa na tija au ufanikiwa. Wakati mwingine maamuzi yanaweza yakawa mazuri au yakaonekana mazuri lakini yasileta matokeo mazuri. Katika mazingira haya kama watu walishikilishwa nafsi mwao watasema “hatujafanikiwa” lakini kama yalikuwa ni maamuzi ya mtu mmoja mathalani kiongozi wao, nafsini mwao watasema “kiongozi hajafanikiwa” na hii husababisha lawama na kufanya kiongozi aonekana si bora.

Dhana ya ‘kiongozi au mtu wa watu’ huzaliwa kwenye namna kiongozi anavyowathamini wafuasi wake na mawazo yao na pia kushirikiana nao. Viongozi wengi wanaopendwa ni wale wenye mahusiano mema na ukaribu na watu wao. Ushirikishaji wengine ni moja ya mambo muhimu sana ya kukonga nyoyo za wafuasi wako na hivyo kuwa kiongozi unayependwa  

Mwisho, ushirikishaji wowote unahtaji busara; kuwa wazi kusikiliza mawazo ya wengine hata kama yanapingana na yako. Lakini pia kuna mazingira ambayo ukiendekeza ushirikishaji wa jumla utachelewa kufanya maamuzi na hivyo kupitwa na fursa. Katika mazingira haya fanya maamuzi na peleka mrejesho wa haraka kwa wafuasi wako ukielezea sababu za kufanya maamuzi peke yako au kwa kushirkisha watu wa chache.

Facebook Comments

Leave a Reply

Be the First to Comment!

avatar