Wajua Kustaafu Kutakuongezea Hatari ya Kifo Usipojipanga?

Picha kwa hisani ya www.askdoctor.com

Katika hali ya kawaida mtu anapomaliza utumishi wake anatakiwa kufurahi kwa sababu maisha baada ya kustafu huonekana kama ni muda mzuri wa kujitua majukumu mengi, kuwa huru na kupumzika. Hakuna haja ya kuamka mapema ili kuwahi kazini, hakuna kukimbizana na ripoti za ofisini wala kupewa maelekezo na bosi wako. Katika nadharia haya ni mazingira ambayo kila mtu huyatamani.

Lakini umeshawahi kujiuliza ajira yako ikikoma kwa sababu yoyote ile utakuwa unafanya shughuli gani? Mathalani, umefukuzwa kazi au muda wa kustaafu umefika nini kitafuata? Kwa walio wengi hili swali huumiza kichwa na muda unapofika na hakuna maaandalizi ya kutosha ni dhahiri msongo wa mawazo hautakuacha salama. 

Tafiti

Tafiti nyingi zinaonesha kuwa watu wengi ufariki muda mfupi baada ya kustaafu. Katika hali ya kawaida mtu anaweza kutetea kuwa hili si jambo la ajabu kwa sababu kadri mwanadamu anavyoongezeka umri hatari ya kupoteza maisha inaongezeka kwa sababu ya uhusiano kati ya uzee na magonjwa na sababu nyingine nyingi.  Utafiti uliofanywa kwa wafanyakazi wa Shell Oil ulibaini kuwa wafanyakazi wanaostaafu wakiwa na miaka 55 wapo kwenye hatari kupoteza maisha ndani ya miaka 10 kwa 89% zaidi ya wale wanao staafu wakiwa na miaka 65. Kwa kifupi, utafiti huu unaonesha kuwa mtu anapo acha kazi mapema anajiweka zaidi kwenye hatari ya kupoteza maisha.

Ripoti ya utafiti iliochapishwa mwaka 2013 na Chuo cha Masuala ya Kiuchumi cha London ilibainisha kuwa kustaafu kazi hunaongeza hatari ya kupata tatizo la sonona kwa 40%. Hili ni moja ya matatizo makubwa sana kwenye afya ya akili na wahanga wa tatizo hili hujikuta wakipata matatizo mengine yanayosababishwa na tatizo hili na hatimaye kupoteza maisha.

Sababu ya hatari ya kifo kuongezeka

Dk. Mziray wa kituo cha afya cha Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi anahusianisha vifo vya mapema vya wastaafu na kukosekana kwa maandalizi ya mapema. Mziray anaongeza kuwa wastaafu wanapomaliza muda wao wanakutana na mahitaji mengi ambayo yanashindwa kutimizwa vyema na kipato cha wakati huo. Hii huleta msongo wa mawazo, shinikizo la damu na baadaye vifo vya mapema.

Ni ukweli ulio wazi kwamba kipindi hiki si rafiki kwa wale ambao wanakuwa hawajajiandaa vyema. Kipato kile ambacho mtu alizoea kukipata kila baada ya muda fulani kinapo ondoka ghafla huku mahitaji yakiongezeka ni dhahiri maisha yanakuwa magumu sana kuyamudu.  Unaweza sema kuwa utalipwa mafao yako na hili ndilo litakuwa suluhisho lakini ukweli ni kwamba  kwa wengi ni suluhisho la muda mfupi sana. Hebu fikiria mfano mdogo tu huu; mwajiri wako anakulipa kiashi cha shilingi 1,500,000/- kwa mwezi unayoitumia kwa matumizi yako kwa mwezi na mara nyingi mishahara uwa haitoshi.  Baada ya kustaafu ukapewa mafao yako ya shilingi 100,000,000/- (milioni mia moja). Kwa haraka haraka hizi ni pesa nyingi sana, waweza sema zitakutosha kumalizia maisha yako yaliyo baki duniani kwa amani. Lakini ukitazama kiuhalisia utagundua hizi si pesa nyingi kama zinavoonekana. Mathalani, utakuwa unatumia kiwango kile kile cha fedha ulizokuwa unatumia kwa mwezi (1, 500,000/-); hii inamaanisha itakuchukua takribani miezi 66 kuzimaliza fedha hizo ambayo ni sawa ni miaka mitano tu. Ninachofahamu ni kwamba kwa watu wengi ukiwa na fedha nyingi kwa wakati mmoja matumizi huongezeka hivyo kwa watu wasio makini fedha hizo zinaweza kuisha hata ndani ya mwaka mmoja. Baada ya fedha kuishi kinachofuata uwa si kitu kizuri.

 Vyanzo mbali mbali vinaonesha kubadilika kwa mfumo wa maisha ni moja ya sababu kuu za kuongeza hatari ya kupoteza maisha. Pamoja na ukweli kwamba ajira ni sehemu ya kupata ujira lakini ni chanzo kikubwa sana cha furaha kupitia wale watu unaokutana nao kila siku. Watu hawa hugeuka kama familia ya karibu unayoshirikiana nayo kwenye mambo mengi na ukishaachana nayo kinachofuata ni upweke unaweza kukuletea sonona (depression).

Ajira pia ni moja ya vitu vinavyofanya miili yetu kuwa imara na hivyo kujikinga na magonjwa mbali mbali. Kuwahi kuamka uwahi kazini na shughuli mbali mbali zinafanya mwili wako kuwa kwenye mjongeo muda wote lakini unapostaafu na kuamua kukaa nyumbani na pengine kuamka muda unaotaka kunaongeza hatari ya kupata magonjwa yanayo ongeza hatari ya kupoteza maisha.

Ushauri

Ni vyema kujiandaa mapema kukabiliana na changamoto za maisha baada ya ajira. Siku ya kwanza niliposaini mkataba wangu wa ajira mzee mmoja alinambia kwa mzaha, “mwanangu, maandalizi ya kustaafu yanaanza leo”. Ukifikiria kauli hii unawezadhani haina mantiki lakini maandalizi ya  kumaliza utumishi wako yanatakiwa yaanze siku unapouanza.

Hii inajumuisha vyanzo vya mapato mbadala ili kuepukana na fedheha ya ukata na kujiandalia makazi mapema na mambo mengine ya kufanya. Usipokuwa makini utamaliza utumishi ndiyo uanze kufikiria kujenga makazi yako hili nalo ni changamoto kwa watu wengi na uwa ni chanzo kikubwa cha kudholotesha afya ya akili.

Kujiuhusisha kwenye shughuli za kijamii kabla na baada ya utumishi kukoma ni jambo la muhimu sana. Hii itakusaidia kuwa na watu wa karibu na kuondoa upweke. Kujihusisha na michezo na kujiunga na vilabu mbali mbali vya kijamii husaidia sana kuondoa upweke na kuushughulisha mwili wako pia.

Jambo la msingi pia ni kuishi na watu vizuri katika ajira au shughuli yoyote unayoifanya. Wakati mwingine msongo wa mawazo huongezeka ukiwaona wale uliowatendea vibaya au kuwanyanyasa wakiendelea na kazi huku wewe utumishi wako ukiwa umekoma nap engine mambo mengine yanaenda kombo. Maneno yatakayo kuwa yakisemwa juu ya matendo yako mabaya uliyoyafanya katika utumishi wako yanaweza kukuumiza zaidi. “Alikuwa anajifanya mbaguzi na mnyanyasaji, kiko wapi sasa, mbona kaicha ofisi?” Wema ni mtaji mkubwa sana maishani.

Facebook Comments

Leave a Reply

1 Comment on "Wajua Kustaafu Kutakuongezea Hatari ya Kifo Usipojipanga?"

avatar
newest oldest most voted
trackback

[…] post Wajua Kustaafu Kutakuongezea Hatari ya Kifo Usipojipanga? appeared first on Kelvin […]