ATHARI YA KUCHAGUA AU KUCHAGULIWA KAZI ISIYO SAHIHI

 

 

 

Picha kwa hisani ya www.lindseypollak.com

Katika kufanya uchaguzi wa nini mtu anataka kufanya hasa kwenye masuala ya ajira sababu hutofautiana. Wapo watu ambao wamechagua fani au kazi fulani kwa sababu tu ndiyo iliyokuwa ikipatikana kirahisi. Lakini pia wapo ambao machaguo yao yaliegemea zaidi kwenye masilahi; hawa walifanya uchaguzi wa kazi fulani kwa sababu tu ina ujira mkubwa. Wengine hawakuchagua kabisa ajira au kazi zao bali walichanguliwa na watu wengine kwa sababu mbali mbali; baba kaja nyumbani na mkataba anakwambia saini hapa kesho utaenda kuanza kazi kama mhasibu katika kampuni fulani.

Kwa sababu yoyote ambayo ilisababisha ukachagua kazi fulani, mwisho wa siku unaweza ukawa umefanya uchaguzi sahihi au usio sahihi. Kuna dalili kadhaa ambazo zinaweza kuonesha dhahiri kuwa kazi yako siyo sahihi. Usahihi unao zungumziwa hapa ni wewe kuendana na kazi husika itakayo kufanya uipende na kuifanya kwa kujitoa na kuifurahia pia.

Unafanya kazi kwa ajiri ya mshahara pekee

Ni dhahiri kuwa mara nyingi ni vigumu sana kwa watu kufanya kazi bila ujira au mshahara. Pamoja na hayo ajira au kazi ina mambo mengine mengi ambayo mfanyakazi anaweza kuyafurahia na yakawa sababu kuifanya kazi kwa moyo ikiwemo kazi yenyewe. Ukiona kuwa unafanya kazi kwa sababu tu unahitaji ujira basi kuna shida sehemu fulani. Matokeo yake ni kufanya kile kitu kiholela na bila kujitoa.

Daktari, anayependa kazi yake hufarijika kuona anaokoa maisha ya wagonjwa wake na kuwarudishia tabasamu. Daktari wa aina hii hujikuta akifanya kazi kwa lengo la kutoa huduma na kufurahia kile anachokifanya. Kama umeshawahi kuhudumiwa na wahudumu tofauti tofauti katika sekta yoyote ile utagundua utofauti kati ya wale wanaofanya kazi kwa ajili ya tumbo pekee na wale ambao wana mapenzi na kile wanachofanya.

Unafurahi kuondoka kazini na kuchukia kuingia kazini

Mara nyingi kazi huchosha akili na mwili na hivyo kuhitaji kupumzika ili kupata nguvu mpya. Pamoja na ukweli huu, ukiona unachukia kile unachokifanya hii inadhirisha pengine ulifanya uchaguzi usio sahihi kuamua kufanya kile unachokifanya. Wakati unafurahi Ijumaa inapofika (Thanks God It’s Friday) na kuichukia Jumapili jioni kila unapokumbuka kesho ni siku ya  kazi, kuna mtu mwingine anatamani Jumatatu ifike ili akatoe huduma. Hii ni kwa sababu anafurahia kile anachokifanya. Kukaa ofisini na kuangalia mshale wa saa huku ukiona kama hausogei kwa sababu unatamani muda wa kutoka uondoke kunaonesha bayana kuwa kazi yako hailandani nawe.

Unajilazimisha kuvaa uhusika usio wako

Kila fani au kazi inamahitaji yake na hii inaenda sambamba kabisa na ukweli kwamba kila kazi inahitaji mtu wa aina fulani. Kwa mfano, watu wanaohusika na mapokezi au huduma kwa wateja ni watu wanaotakiwa kuwa wachangamfu, wenye lugha nzuri na tabasamu linaweza kukufanya uendelee kuwasikiliza. Watu wasio na sifa hizi wakati mwingine hujikuta wakitoa huduma ya aina hii ni rahisi kugundua kwamba wao ni waigizaji tu na hakuna cha maana wanachofanya. Hali hii ipo kwenye fani au kazi nyingi sana na uwakumba watu wanaolazimika kuvaa uhusika usio kuwa halisi.

Unapata mrejesho mbaya mara kwa mara

Kile tunachokifanya katika kazi zetu huleta matokeo kwa wadau mbali mbali; wateja, wafanyakazi wenzetu, mabosi wetu na wengine wengi. Mrejesho wa matokeo ya kile unachokifanya kutoka kwa wadau hawa unaweza kukufanya kugundua kama kazi yako ni sahihi au si sahihi. Endapo utagudua kuwa pamoja na muda mwingi uliofanya kazi lakini bado unapata mrejesho mbaya mara kwa mara  kutoka kwa watu mbali mbali hii ni dalili kuwa kuna shida kwenye uchaguzi wa kile unachokifanya sasa. Ukisikia  wateja wanasema hawafurahii wanapohudumiwa na wewe basi kuna haja ya wewe kuanza kujihoji.

Unahisi ujuzi na uwezo wako hautumiki ipasavyo

Kila kazi inahitaji kiasi fulani cha ujuzi na pengine uzoefu ili ifanywe vizuri. Wakati mwingine unaweza kuwa unafanya kazi lakini unahisi kile ulichonacho ni kikubwa sana ukilinganisha ni kile unachokifanya. Hili suala wakati mwingine linahitaji tu kutathmini majukumu yako na kuyaongezea ukubwa ili yaweze kuwiana au kuzidi ujuzi ulionao. Lakini mara nyingi tatizo linakuwa siyo tu ile nafasi uliyopewa bali na kazi nzima kwa ujumla. Endapo unahisi hali kama hii ni moja ya dalili kuwa kazi yako hailandani na wewe au uwezo wako.

Fikra kwamba hauna mchango kwenye taasisi

Mara nyingi taasisi uwa na watu tofauti wenye uwezo tofauti pia. Utofauti huu hufanya kila mtu ahitajike na athaminike  kutokana na kile anachokifanya kuleta tija katika maendeleo ya taasisi. Hii ina maanisha endapo mtu huyo kwa sababu yoyote hatakuwepo eneo la kazi basi pengo lake lazima litaonekana. Kwa wengine hali huwa tofauti; unapogundua kuwa uwepo wako hauleti tofauti yoyote au hauchangii chochote kwenye maendeleo ya taasisi au kutokuwepo kwako hakuleti shida yoyote kazini kwako  kuna uwezekano kabisa upo sehemu isiyo sahihi.

USHAURI

Inawezekana kabisa umeshaona baadhi ya dalili hizi kwenye kazi yako. Kuwa sehemu isiyo sahihi inaweza ikawa ndiyo sababu ya msingi. Hili lisikuumize kichwa, shida inaweza isiwe aina ya kazi au fani, mathalani uhasibu lakini shida ikawa ni majukumu uliyopewa ndiyo yanasababisha uone kuwa hauendani na kazi hiyo. Sababu za hali hii zinaweza kuwa nyingi na pengine ni aina ya watu unaofanya nao kazi. Si vyema kukaa kimya unapojisikia kuwa na hali hii; zungumza na mtu unayedhani atakusaidia.

Endapo kazi unayoifanya ilikuwa ni kwa muda tu pengine ili uweze kukidhi mahitaji yako, mathalani ya kifedha ni vyema kutafuta kazi unayodhani itakupa utoshelevu, utaifurahia na utaipenda. Maisha yetu kwa sehemu kubwa tunayatumia katika kufanya kazi, usikubali kufanya kazi inayokutesa na uifurahii kwa sababu itakuongezea msongo wa mawazo na kuleta athari nyingine za kiafya. Fanya kile unachokipenda, hautachukulia kazi kama adhabu.

Mwisho, ikumbukwe kuwa sababu hizi zisitumiwe kujitathmini na watu ambao ni wavivu kiasikli au kwa makusudi. Kama wewe ni mvivu na ukaamua kutokujituma hakuna kazi itakayo kuwa sahihi kwako.

Facebook Comments

Leave a Reply

1 Comment on "ATHARI YA KUCHAGUA AU KUCHAGULIWA KAZI ISIYO SAHIHI"

avatar
newest oldest most voted
trackback

[…] post ATHARI YA KUCHAGUA AU KUCHAGULIWA KAZI ISIYO SAHIHI appeared first on Kelvin […]