Mambo 6 ya Kuzingatia Unapochagua Fani au Kazi

Maisha yetu ya sasa na ya baadaye ni matokeo ya maamuzi tunayo yafanya sasa au tuliyo yaliyoyafanya kipindi cha nyuma. Kufanya maamuzi sahihi ni jambo muhimu pengine kuliko yote katika kufikia malengo na mafanikio yetu.

Katika masuala ya ajira na kazi wengi wamejikuta wakijutia maamuzi ambayo wamekwisha yafanya. Kitu kibaya kuhusu ajira, kazi au hata taaluma ambayo mtu ameisomea yanaweza yakamfanya akawa mtu mtumwa wa shughuli au kazi fulani asipokuwa makini.

Mara kadhaa nimekuwa nikiwashauri vijana wanaponiuliza maswali kama nisome kozi gani inayolipa zaidi? ipi itanifanya nipate ajira kwa haraka? Nimepata kazi sehemu zaidi ya moja nichague ipi? Mengi ya maswali ambayo vijana uniuliza yana ashiria mambo makubwa mawili. Moja, wengi hawana taarifa za kutosha na pili, hawajajiandaa kikamilifu na hivyo hawajui wafanye nini. Hili la pili pengine linasababishwa na la kwanza.

Kuna baadhi ya mambo ambayo ni ya msingi sana kuyazingatia  unapoamua kuchagua fani au kazi ya kufanya;

  1. Nini Unapenda

Kwa bahati mbaya watu wamekuwa wavivu wa kujitathmini kujua nini wanapenda kufanya lakini pia hata kwa wale wanao jua hawadhani kuwa hili ndilo jambo kubwa zaidi la kuzingatia pengine kuliko yote mtu anapoamua kuchagua fani au kazi ya kufanya na makossa mengi hufanyika katika kigezo hiki.

Watu wanaofanya shughuli zao vizuri na kwa kujituma ni wale wanaofanya kile wanachokipenda hata kama kina ujira mdogo. Watu hawa utawatofautisha na wengine kwa jinsi wanavyotoa huduma. Kama unapenda kuwa mwalimu, muuguzi, askari, daktari  usijilazimeshe kufanya kingine ambacho haukipendi kwa sababu madhara yake ni makubwa sana baadaye hata kama kina ujira mdogo.

  1. Haiba yako

Moja ya vitu ambavyo pengine watu huacha kuvizingatia na kuwaletea madhara baadaye ni haiba (personality). Tafiti zinaonyesha ufanisi na utoshelevu au furaha ya kazi huendana na haiba ya mtu. Kuna baadhi ya kazi zinahitaji watu waongeaji, wanaojichanganya na wasio na aibu, mathalani afisa uhusiano. Ukiwa mkimya, mpole na pengine muoga ukichagua fani ya aina hii itakuwa ngumu kupata ajira kwani watakapo kufanyia tathmini kwenye usaili wa kazi utaonekana haufai na endapo utaaipata kazi hiyo hauta ifurahia kabisa.

  1. Ujuzi na vipawa ulivyonavyo

Katika maisha ya kila siku tunaongeza ujuzi katika kufanya mambo tofauti tofauti. Pengine, katika kuzungumza na watu unaweza jikuta unauwezo mzuri wa kushauri na watu wakawa wanafurahia na kuridhika kila unapozungumza nao. Unachoweza kuwa unakosa pengine mafunzo kidogo tu kuifanya shughuli hii kwa ufanisi zaidi. Hili pia ni suala la kuzingatia unapoamua kuchagua nini ufanye kwani kinadhirisha kile ambacho unaweza kukifanya tayari.

Pia kuna watu wengine kiasili wanavipawa fulani ambavyo vinaweza kuwasaidia katika kucgaua nini wafanye. Wapo watu ambao ukiwasikia tu wakiongea utandua wana kitu ndani yao ambacho wakikifanya kiuledi kitawafanikisha na kuwafikisha mbali.

  1. Vipaumbele katika maisha yako

Kila mtu anavitu ambavyo anivithamini zaidi katika maisha yake na hivyo kuvipa kipaumbele katika kila anachokifanya. Wapo watu ambao masuala ya imani au dini ni vitu ambavyo wanavithamini sana, wengine michezo, huku wengine wakitoa kipaumbele zaidi kwenye familia zao hivyo kutamani wawe na muda wa kutosha na familia zao. Katika kuchagua fani au kazi yoyote ni muhimu kuzingatia haya kwa sababu kuna siku au pengine mara zote kazi yako itaingiliana na vipaumbele vyako.

  1. Mafunzo

Fani nyingi zinaahitaji mafunzo ili kuweza kuzimudu na kuzifanya kwa ufanisi na ufasaha. Ni vyema kutathmini aina ya mafunzo, matakwa ya mafunzo hayo na muda wa mafunzo stahiki ili kuona kama utaweza ya mudu. Kama unataka kuwa daktari ni vyema kujua mahitaji ya mafunzo ya udaktari ili kuona kama una sifa stahiki. Kujua fani unayotaka kuichagua mapema kutakuwa msada mkubwa katika kujiandaa na kuwa na sifa za awali kabla ya kuingia kwenye mafunzo ya fani husika.

Kwa mfano, mtu ambaye angependa kuwa mhandisi wa barabara akiwa sekondari ana nafasi kubwa ya kutafuta sifa za awali hasa katika kuchagua masomo (mchepuo) kabla ya kwenda chuo kusomea fani hiyo.

  1. Mazingira ya kazi

Suala la mazingira ya kazi ni suala pana sana likijumuisha kazi yenyewe na mambo yanayo ambatana na kazi hiyo. Hii inajumuisha ujira, majukumu, lengo la kazi yenyewe na mengineyo mengi.

Mazingira ya kazi ya afisa wa benki yanatofautiana kabisa na yale ya mwalimu. Kwa kuzingatia sababu nyingine zilizotajwa juu na kutathmini mazingira ya kazi yenyewe itakusaidia kuona kama utaweza imudu fani husika au vinginevyo. Kazi nyingine zinahitaji kuwa chini ya uangalizi na usimamizi muda wote na wengine hawako tayari kwenye hili.

Changamoto

Katika uchaguzi wa fani watu wengi wamekumbana na changamoto kadhaa, moja ikiwa kushindwa gharama za fani husika ambayo pengine mtu anaipenda. Changamoto nyingine ni kutumia sababu za muda mfupi kufanya maamuzi yenye athari za kudumu. Kwa mfano, wapo walioamua kusomea shahada ya ualimu kisa tu serikali ilikuwa ikitoa mikopo kwa wanafunzi wa shahada ya ualimu lakini pia wakihitimu hupangiwa vituo vya kazi.

Katika changamoto ya kwanza, mtu anaweza kuangalia vyanzo mbali mbali vya kukusanya fedha ikiwa ni pamoja na ndugu, jamaa na marafiki lakini pia kuangaliza fursa za ufadhili ndani na nje ya nchi.

Changamoto ya pili ni mtego wa kuuepuka pale inapowezekana. Hebu fikiria, umesomea fani fulani sio kwa mapenzi yako lakini tu ili upangiwe kituo na serikali baada ya kuhitimu halafu serikali ikathitisha utaratibu huo ukiwa unaendelea na masomo au mara tu baada ya kumaliza masomo yako.

Hata ukipata ajira kama sio fani uliyoipenda ni dhahiri utakuwa mtumwa wa kazi hiyo kwani utakuwa unafanya kitu usicho na amani nacho. Hii itaathiri ufanisi na utendaji wako kazini

Facebook Comments

Leave a Reply

Be the First to Comment!

avatar