Tabia 9 Zinazoweza Kukufanya Ufurahie Ajira Yako

Kila mtu anapenda kufurahia kile anachokifanya. Furaha ni moja ya misigi ya utendaji mzuri na ufanisi katika shughuli yoyote ile. Kwa bahati mbaya watu hujikuta wanapoteza furaha ile waliyokuwa nayo katika ajira zao na mwisho kuchukia kazi wanazofanya.

Sababu za kukosa furaha katika ajira ni nyingi sana. Nyingine uhusiana na kushindwa kufikia malengo, mazingira ya kazi, mahusiano kati ya mwajiriwa na mwajiri na wakati mwingine watu wengine mahala pa kazi. Wakati mwingine sababu zinaweza zikawa ni zile zisizohusiana na ajira moja kwa moja. Majukumu yanapoongezeka yanaweza kufanya ukaichukia ajira yako kwa sababu ujira unaopata haukidhi mahitaji yako na hivyo unaona kama ajira yako yaitoshelezi au haifikii malengo yako.

Mahusiano na watu wengine nje ya ajira yako yanaweza kuwa chanzo cha msongo wa mawazo unaoweza kupelekea kukosa furaha ukiwa kazini.

Kuepuka hali hii unaweza kujenga tabia zifuatazo zinazoweza kukusaidia kuongeza furaha katika ajira yako;

  1. Kujifunza

Mara nyingi sababu kubwa ya kutofanya vizuri au kuwa na utendaji mbaya kazini ni kukosa mbinu au uwezo wa kuifanya kazi husika. Hii husababisha watu kukosa furaha kwenye ajira zao. Ni vyema kujenga tabia ya kujifunza mara kwa mara ili kupata ujuzi na mbinu bora za kufanya kile unachokifanya. Kujifunza kunaweza kuwa kupitia mafunzo rasmi lakini wakati mwingine kupitia watu wenye ujuzi ambao wewe hauna.

Omba watu wa kufundishe, soma vitabu, tumia mtandao wa intaneti vizuri, soma makala mbali mbali na mambo mengine yanayoweza kukufanya uwe uwezo na ujuzi zaidi.

  1. Onyesha upendo

Watu wenye tabia ya kupenda wengine uishi kwa furaha. Na hii si makazini tu bali kila mahali. Ukionyesha chuki unatengeneza mazingira ya kuumia baadaye. Wapo watu wengine ambao kwa makusudi uwachukia wengine na kutamani wasifanikiwe kabisa. Wakati mwingine watu hawa uishia kutafuta mbinu za kuwakwamisha wengine kwa makusudi kwani kushindwa kwao ndiyo furaha kwao.

Hii huwasababishia maumivu pale wanapoona watu hao wamefanikiwa. Kwa nini ujitesa kisa roho mbaya? Jenga tabia kupenda na kuuonesha upendo kwa watu wote ili wanapoinuka iwe furaha kwako pia na maisha yaendelee.

  1. Ongeza mtandao wa kiajira wenye tija

Fursa nyingi hupatikana kupitia watu wetu wa karibu. Hawa ni marafiki tunaowachagua miongoni mwa wengi. Hakikisha unatengeneza mtandao wa watu wanaoweza kuwa msada kwako kwa namna tofauti tofauti nje na ndani ya mahala unapofanyia kazi. Ofisini kwako mkitembelewa na mtu kutoka makao makuu, ukipata fursa ya kuongea naye usimwache aondoke bila hata kuchukua mawasiliano yake. Jenga urafiki wenye maana unaoweza kuwa msada sasa na hata baadaye.

Watu wenye mtandao wa kiajira wenye tija mara nyingi uwa na furaha kwani kupitia mitandao yao wapo washauri wa kuwasaidia pale inapobidi lakini pia kuwaonyesha fursa za kiajira na hata zisizo za kiajira zinazojitokeza.

  1. Jenga na linda afya yako

Miili na akili zetu inatumika sana kwenye shughuli za kila siku. Inapoathirika shughuli nyingi zinakwama na kutufanya watu tusiofurahia kile tunachokifanya. Kumbuka kuhakikisha unaijenga na kuilinda afya yako. Wahi kulala na wahi kuamka pia, fanya mazoezi, kula vizuri, punguza matumizi ya vileo yaliyopitiliza na ukiweza acha kabisa, chunguza afya yako mara kwa na kupata matibabu kwa wakati pale yanapohitajika.

Watu wengi hulalamika kuwa kazi zinawapa msongo wa mawazo na magonjwa mengine mengi. Wakati mwingine hii husababishwa na kutozingatia mambo niliyo yataja hapo juu.

  1. Kuwa na nidhamu

Mara nyingi migogoro mahala pa kazi husababishwa na watumishi kuwa na utovu wa nidhamu. Hii upelekea watu kukosa amani na kuchukia kazi zao. Nidhamu ni tabia kwa sababu hupimwa kutokana na yale tunayosema na kutenda. Kuwa na tabia njema kwa kila mtu na heshimu sheria, taratibu na miongozo utajiepusha na matatizo mengi na kufurahia ajira yako.

 

  1. Weka mipango katika shughuli zako

Watu wanaopanga mambo yao vyema hujiepusha na matatizo mengi. Hakisha unapanga mambo yako na kujiandaa vyema kutekeleza mipango yako. Hakikisha kabla haujaenda kazini unajua ni nini utafanya siku hiyo na utahitaji rasilimali zipi. Usifanye mambo mengi kwa wakati mmoja, maliza jambo moja kisha fanya jingine. Hakikisha mambo mengine hayavurugi ratiba zako na endapo majukumu ni mengi usisite kuomba msada kwa wengine pia.

  1. Jipende

Pamoja na kujenga tabia ya kuwapenda wengine hakikisha unajipenda kwanza. Hii itakusaidia kuongeza thamani yako kwanza na kisha kwa wengine pia. Kumbuka kupendeza na kuwa nadhifu na wakati mwingine kujikumbusha kuwa unajipenda; si mara zote wanaokupenda watakwambia. Ofisi yako iwe safi pia; itakufanya ufurahie kuwepo hapo na kuifurahia kazi yako.

  1. Kuwa mkweli na muwazi

Kuna kitu hakijakufurahisha, sema. Unahisi majukumu uliyopewa ni mengi, usikae kimya. Bosi wako kakukwaza, usibaki na kinyongo. Maisha haya ni mafupi sana hivyo usikubali mtu mwingine akawa kero na wewe ukakubali kuumia. Kuna baadhi ya watu wako tayari kudanganya ili kuwafurahisha wngine huku wao wakiumia-huu ni utumwa. Ukweli utakuweka huru. Pamoja na hayo kumbuka kutumia busara katika kuelezea fikra na mitazamo yako kwa mtu yoyote yule awe na cheo, asiwe na cheo, awe mkubwa au mdogo.

  1. Weka uwiano mzuri wa ajira na maisha binafsi

Ajira ni muhimu sana katika maisha lakini kuna maisha baada ya ajira ambayo nayo ni muhimu pia. Ajira iaathiri maisha binafsi na maisha binafsi nayo yana athiri ajira zetu hivyo ni muhimu kuweka uwiano mzuri kati ya mambo haya mawili. Ajira isifanye ukose muda wa kwenda kwenye nyumba za ibada, kukaa na familia, kukutana na marafiki na jamaa zako. Lakini pia vitu hivi viwe kwa kiasi visije kuletea shida kwenye ajira yako.

Facebook Comments

Leave a Reply

Be the First to Comment!

avatar