JINSI YA KUTENGENEZA MTANDAO BORA WA AJIRA NA BIASHARA

Shughuli nyingi duniani zinafanikiwa kwa kutegemeana. Hauwezi kufanikiwa kwa kuamua kufanya kila kitu peke yako pasipo kuwashirikisha au kujifunza kutoka kwa wengine. Hii inatulazimu kuhakikisha tunatengeneza mitandao ya watu watakao kuwa na tija kwenye mafanikio ya shughuli zetu.

Kila siku kuna jambo jipya la kujifunza linaloweza kukusogeza hatua moja mbele katika mafanikio ya kile unachofanya. Njia nzuri ya kujifunza ni kuwa karibu na wale waliofanikiwa tayari. Lengo la kutengeneza mtandao wa kiajira au biashara siyo kujifunza pekee bali kupata fursa mbali mbali zinazoweza kuwa matokeo ya kuwa karibu na wale wanaoweza kuwa msaada katika kukupa fursa mbali mbali ikiwemo taarifa.

Wewe kama ni mfanyabiashara kuna wafanyabiashara wengine ambao wanaweza kusadia biashara yako kwa namna moja ama nyingine. Hawa ni watu kuwaweka karibu sana. Kama unatarajia kufanya kazi kampuni fulani hapo baadaye ni vyema kutafuta mtu au watu wanaoweza kuwa msaada kufikia lengo hilo.

Mtandao wa kiajira au kibiashara ni jumla watu wako wa karibu unaowasiliana nao mara kwa mara huku uhusiano wenu ukiwa umejengwa kwa lengo la wewe kunufaika au kunufaishana katika shughuli mnazofanya au mnazotarajia kufanya.

Je, ni nani wa kumuweka kwenye mtandao wako?

Sio kila mtu anastahili kuwa kwenye matandao wako. Kuna mambo kadhaa ya kuzingatia unapoamua kumuingiza mtu kwenye aina hii ya mtandao lakini kigezo kikubwa ni mtu anayaweza kukupa fursa au mwenye uwezo wa kukuunganisha na fursa au watu wengine wenye fursa au yeye mwenyewe ni fursa katika mafanikio ya shughuli zako. Usimuweke mtu kwenye mtandao wako ambaye si msaada na wala hatakuwa msaada katika shughuli zako sababu mwisho wa siku anaweza kuwa mzigo pia.

Ukiwa unatamani kuwa mshehereshaji (MC) mwenye mafanikio ni vyema kuanza kufanya utafiti ili kujua ni watu gani wamefanikiwa katika eneo hili na kuwaweka karibu. Wakati mwingine itakubi kuwaomba ufanye nao kazi hata bila malipo ili uweze kujifunza na kuunganishwa na watu wengine wanaoweza kuwa msaada katika shughul hii.

Mbinu hii inawafaa sana wale walio kwenye mchakato wa kutafuta ajira. Ni vyema kuwa karibu na wale wanaoweza kuwa ngazi ya mafanikio yako kama siyo sasa basi ni ya baadaye.   

Unawezaje kuwapata watu sahihi wa kuwaweka kwenye mtandao?

Kile unachokifanya au unataka kukifanya mara nyingi kinakuwa tayari kimeshafanywa na watu wengine na wameshafanikiwa kwa kiasi kikubwa. Ukitaka kuanzisha biashara ya kuafirisha nafaka kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine wapo watu wamekuwa wakiifanya biashara hii kwa miaka mingi na wana uzowefu. Tafuta wawasilino yao na omba kuonana nao ana kwa ana kama inawezekana.

Kama ni ngumu kuonana nao zungumza nao kwa simu au barua pepe ukieleza lengo la wewe kutaka kujifunza kutoka kwao. Inawezekana wapo wanaoweza wasipende wazo hili lakini pia wapo wanaoweza kuonesha moyo wa kusaidia.

Katika masuala ya biashara wateja wako wa sasa na wateja wako watarajiwa ni watu muhimu sana kuwaweka karibu ili wawe msaada kwenye biashara yako. Wapo wafanyabiashara waliojiwekea utaratibu wa kuwajulia hali wateja wao na kufanya ufuatiliaji wa mrejesho wa huduma au bidhaa wanayo uza.

Kumbuka ni vyema  kuwa mtu wa kujichanganya na kujitambulisha kwa watu tofauti ili wajue unafanya shughuli gani na kama ni mtafuta ajira wajue sifa ulizo nazo. Umeenda kwenye kongamano na umekutana na watu mbali mbali, wasalimie, ongea nao ili ujue shughuli waazofanya na mwisho ubadilishane nao mwasiliano na ukumbuke kuwasiliana nao muda mfupi baada ya kuachana nao.

Jinsi ya kuimarisha mtandao wako

Unapoamua kuanzisha mtandao au kumuweka mtu kwenye mtandao wako ni vyema kuzingatia kuwa ili mtandao uwe na tija ni lazima uimarishwe. Njia kuu ya kuimarisha mtandao wa aina hii ni mawasilinao ya mara kwa mara. Mawasiliano haya yanaweza kuwa kwa njia ya simu, barua pepe na njia nyingine za mawasilinao lakini kukutana ana kwa ana pale inapowezekana.

Wasiliana na wadau wako hasa wateja. Unaweza jiuliza, kama nina wateja wengi sana huo muda wa kumjulia hali mmoja mmoja au kujua kama wamelidhika na huduma ua bidhaa yangu nitautoa wapi? Si lazima ufanye wewe lakini pia teknolojia imerahisisha mawasilino kwani waweza tuma barua pepe moja kwa mamia ya wateja wako au kwa kuwatumia ujumbe mfupi wote kwa pamoja.

Kwa wale wadau wako wakuu au wa karibu sana ni vyema kufanya mawasilino ya moja kwa moja na ikiwezekana kukutana nao mara kwa mara.

Suala jingine ni kuhakikisha kuwa unakuwa mwaminifu. Si vyema kutoa taarifa za uongo na ahadi usizowezo kuzitekeleza. Mambo haya yana athari kubwa sana katika mtandao na yanaweza kukuharibia sifa njema na kuondoa imani kutoka wadau mbali mbali.

Angalizo

Kwa kuzingatia kuwa mawasiliano ndiyo msingi wa mtandao bora ni vyema kuhakikisha kuwa mawasiliano yanafanywa kwa uangalifu. Watu hututathamini kwa namna tunavyowasiliana nao. Hakikisha kuwa mawasilino yako hayawi kero au usumbufu kwa watu kwenye mtandao wako.

Ni vyema kuzingatia muda wa kufanya mawasilino; si kila wakati ni muda muafaka wa kufanya mawasilino. Wapo ambao hawapendi kufanya mawasiliano usiku wanapokuwa na familia zao na hupenda kufanya hivyo muda wa kazi pekee.

Mtandao bora ni ule ambao ni kutegemeana na siyo wa kunufuisha upande mmoja hivyo ni vyema kuhakikisha unajitahidi kuangalia mtandao wako utawanufaishaje watu kwenye mtandao wako. Inawezekana hauwezi kutoa ajira lakini unaweza kutoa taarifa zinazoweza kuwa msaada kwa watu wengine kwenye mtandao wako.

Facebook Comments

Leave a Reply

Be the First to Comment!

avatar