MAMBO 10 YA KUZINGATIA UWE KIONGOZI UNAYEPENDWA MAHALA PA KAZI

Malalamiko na migogoro mingi maeneo ya kazi yamekuwa yakisababishwa na mahusiano yasiyofaa ndani ya taasisi hasa kati ya viongozi na wafuasi wao. Mahusiano yasiyofaa yamekuwa changamoto kiasi kufikia watu wengine kuchukia kazi zao na kufikia hata kuacha ajira zao.

Wapo viongozi ambao kwa makusudi hugeuka kero kwa wengine. Kila mtu anatamani mahala pa kazi pawe ni sehemu salama panye furaha wakati wote. Unyeyekevu ni kitu ambacho kinaweza kuwa dawa ya migogoro mingi na kufanya watu wawe watiifu kwa viongozi wao na kufanya taasisi ziwe mahala zenye furaha.

Kuna mambo kadha viongozi anaweza kuyafanya, akaendwa na yakamuwezesha kuwa kimbilio na chanzo cha furaha.

  1. Kuwa Msikivu

Watu wengi hupenda kuongea zaidi ya kusikiliza na kuonekana wanatawala mazungumzo au mawasiliano. Hii husababisha wengine kuwaona kama ni watu wanaojifanya wanajua sana na kusababisha kutokuonekana kutengeneza mazingira yasiyo rafiki. Jifunze kusikiliza zaidi ya kuongea. Na hii ni sifa muhimu kwa viongozi.

  1. Kubali unapofanya makosa

Kila mtu hukosea wakati fulani. Kwa bahati mbaya wapo ambao hawapendi kuonekana si wakamilifu. Ni vyema kukiri unapofanya kosa na siyo kutafuta mtu wa kumpa lawama. Hii itaonesha utayari wako wa kuwajibika na kujifunza pia. Watu wasio wanyenyekevu wanatabia ya kujiona si wakosefu na kila wanachofanya kiko sawa.

  1. Wasiliana vyema

Mawasiliano ni moja ya vitu vinavyo iweka taasisi pamoja na kama kiongozi ni jukumu lako kuhakikisha kuwa mawasiliano yanafanyika vizuri na kwa wakati. Zaidi ya hili wewe kama kiongozi unatakiwa kuhakikisha unawasiliana vyema na wengine. Hakikisha unatumia njia sahihi za mawasiliano na unawasilina kwa wakati. Viongozi wengi hukosea kwenye kauli zao; suala siyo unaongea nini lakini unaongeaje. Kuwa na lugha za staha ambazo hazita kuwa kero kwa wengine.

  1. Pongeza inapobidi

Watu wanapofanya vizuri kwenye jambo fulani hutarajia kutiwa moyo na kupongezwa. Usijifanye hauwaoni au hautambui mambo mazuri wanayoyafanya; chukua muda kuwapongeza ana kwa ana na mbele ya wengine. Inapotokea mtu amefanya vibaya tafuta njia ya kumrekebisha kwa upendo. Si vyema kumsema au kumkosoa mtu mbele ya kadamnasi hasa kwa makosa kiutendaji ambayo pengine yamesababishwa na kukosekana kwa muda, rasilimali na pengine mafunzo. Kiongozi anataliwa kuwa kama mzazi; anapongeza (kwa moyo wake wote), anakosoa (kwa staha), ana adhibu (kwa utaratibu) lakini pia anakuwa kimbilio na siyo wa kukimbiwa.

  1. Kumbuka hautakuwa ulipo milele

Nyandhfa na vyeo huwapa watu kiburi na kujikuta wanasahau kuwa nafasi walizopewa ni dhamana na baada ya muda hawatakuwa nazo tena. Kukumbuka ukweli huu itakufanyau uwapende wengine, kutenda haki na kupendwa na wafuasi wako. Ukifanya kinyume na haya siku utakapomaliza muda wa kutumikia cheo chako au nyadhfa uliyonayo kwa sababu yoyote ile itakupa shida zitakazo kuletea msongo wa mawazo na kukosa amani.

  1. Usijifikirie wewe tu, wakumbuke wengine

Kiasili sisi binadamu ni wa binafsi lakini wapo ambao kiwango cha ubinafsi kimefika viwango vya kutafsiriwa kama chuki. Maamuzi mengi tunayofanya tunaangalia maslahi yetu kwanza bila kuyazingatia ya watu wengine. Viongozi mara nyingi hupewa upendeleo au maslahi ya tofauti ukilinganisha na yale ya watendaji wengine. Hii uwafanya wasahau kabisa mahitaji ya watu wengine hasa wale wasionufaika kama wao.

Kabla haujafanya, sema au kuwaza mambo ya usuyo taasisi yako chukua muda wa kuwa kwenye nafasi za wale unaowaongoza. Mbaya zaidi ni ukweli kwamba wale ambao uwa wahanga wa maamuzi mabaya na kulalamika wakishapata nafasi za uongozi huyafanya yale yale waliyokuwa wakiyalalamikia pindi walipokuwa wakifanyiwa. Na hata wale waliosaidiwa kufika hapo hukosa muda wa kuwasaidia wengine.

  1. Jichanganye

Uongozi hautakiwi kuwa ukuta bali daraja la kukuunganisha na wafuasi wako. Kisa umepata cheo ndiyo hautaki hata kupita ofisini kutusalimia kama zamani? Tulikuwa tunapata chakula pamoja lakini siku hizi hata misibani wala harusini hautaki kuudhuria. Hii itakuharibia sifa njema; jichanganye tu, haitashusha hadhi yako bali itakuweka karibu zaidi na watu wako. Watu wazoee ukaribu wako, siyo ukipita mahali watu wananyamaza kwa hofu kiongozi anatakiwa kuwa rafiki. Matukio ya kitaasisi hata kama ni ya idara fulani hebu jitokeze kushiriki.

  1. Kuwa kiongozi wa mfano

Moja ya changamoto kubwa katika uongozi ni watu kusema kile wasichofanya. Kama kiongozi unaosisitiza uaminifu, upendo, ushirikiano na mengineyo usiishie tu hapo. Mambo haya yanatakiwa ya akisi katika maneno, mawazo na matendo yako mahala pa kazi. Kiongozi bora ni yule anayeishi maneno yake. Kumbuka kushiriki moja kwa moja kwenye shughuli za taasisi pale inapobidi. Usiseme tu hebu fanyeni hili lakini sema hebu tufanye hili ili kuonekana kuwa wewe ni mmoja wa timu.

  1. Usibague

Binadamu wengi tunatabia ya kuwa na uendeleo. Hili si suala baya nan i asili yetu. Kwa sababu fulani unampenda mtu au watu fulani hivyo kujikuta unawaweka karibu au kuwapa fursa zaidi ya wengine. Hii si tabia kwa viongozi wa watu. Kwa kifupi haitakiwi kwa viongozi mahali popote kuwa na sifa hii. Usiwagawe wafuasi wako bali uwe sababu ya kuwaunganisha na ndiyo jukumu la kiongozi.

  1. Tekeleza ahadi zako

Ukiona hauwezi kulifanikisha jambo fulani basi usiwe na haraka kuliahidi. Moja ya sifa kuu ya viongozi bora ni kuwa waaminifu. Mambo yanayovunja uaminifu kwa wafuasi wako kama ahadi zisizo tekelezeka ni ya kuyaeuka kabisa. Cha msingi ni kuhakikisha una kumbukumbu sahihi ya kila ahadi uliyoitoa au mipango ya taasisi na kuhakikisha vinatekelezwa kwa wakati.

Mwisho, kumbuka hauwezi kupendwa na kila mtu. Lengo lisiwe kutafuta kupendwa bali kutekeleza majukumu yako huku ukizingatia taratibu, sheria na miongozo. Ila kuyafanya haya vyema unahitaji kuweka mazingira mazuri kati yako na unaowaongoza na hapo upendo ndiyo nguzo. Kumbuka, hauwezi kupendwa kama haupendi.

Facebook Comments

Leave a Reply

1 Comment on "MAMBO 10 YA KUZINGATIA UWE KIONGOZI UNAYEPENDWA MAHALA PA KAZI"

avatar
newest oldest most voted
trackback

[…] post MAMBO 10 YA KUZINGATIA UWE KIONGOZI UNAYEPENDWA MAHALA PA KAZI appeared first on Kelvin […]