TABIA ZA KUEPUKA ILI KUIMARISHA MAHUSIANO KAZINI

 

Mafanikio katika sehemu yoyote ile hufikiwa kwa jenga tabia fulani zinazoweza kukufanya uwe bora zaidi. Pamoja na kujenga tabia fulani bado unahitaji kuziepuka baadhi ya tabia ili kufikia malengo yale yale uliyojiwekea. Katika masuala ya ajira na kazi nako kuna tabia za kuzijenga na nyingine za kuzibomoa na kuziepuka kabisa. Imekuwa kawaida kwa watu wengi kusisitiza tabia ambazo watu wanatakiwa kujenga ili kuongeza ufanisi katika mambo mbali maeneo ya kazi. Leo tuangazie tabia ambazo hazitakiwe kupewa nafasi kabisa ili ujenge na kuimarisha mahusiano mazuri na wafanyakazi wenzako maeneo ya kazi

KUJIPENDEKEZA KWA MABOSI

Moja ya vitu vinavyoweza kufanya ukachukiwa na kutengwa na wafanyakazi wenzako ni kujipendekeza kwa mabosi kwa nia mbaya. Imekuwa desturi kwa baadhi ya watu kuamua kuwa karibu na viongozi au mabosi wa taasisi kwa lengo la kupata upendeleo wa mambo fulani au pengine kuonekana wao ni bora zaidi. Mara nyingi hii siyo shida kubwa lakini pale ambapo kujipendekaza huku kutaendana sambamba na kuharibu sifa za wengine hakika hili si jambo la kiungwana kabisa. Ili kudhihirisha kwamba wewe ni mzuri haina haja ya kusema fulani ni mbaya. Imekuwa kasumba ya baadhi ya watu kuwasema vibaya wengine kwa viongozi wakidhani hili suala litawainua wao.

Ni vyema kukumbuka kuwa tabia hii ina madhara makubwa kwani wale unaojipendekeza kwao hawatakuwepo hapo milele na wale ambao unawakandamiza na kuharibu sifa zao wanaweza kuja kuwa mabosi wako kesho na ukashindwa pa kukimbilia.

KUWA MTU WA KUONA MAKOSA PEKEE

Kila mtu ana mambo mazuri na mabaya anayoyafanya iwe kwa ajili yake au watu wengine. Kwa bahati mbaya wapo ambao ufumba macho kwa yale mazuri na kuyaona mabaya pekee kwa watu wengine. Watu hawa hutumia vinywa vyao kukosoa yale wanayoyafanya wengine.  Pia, watu hawa udharau uwezo wa wengine na kuwa na mitazamo hasi juu yao. Tabia hii si njema na haifai kuwepo katika sehemu za kazi. Tujifunze kuwa watu wa kutia moyo wengine kwa yale wanayoyafanya na hata pale inapobidi kukosoa ni vyema kulifanya hili kwa staha. Kila mtu ana kitu kizuri tunachoweza kukisemea kwa wengine, tunaweza kuchagua sifa njema na kusihubiri kwa wengine na wala siyo zile mbaya pekee.

UBINAFSI

Taasisi ni muunganiko wa watu wanaofanya kazi kwa pamoja huku wakitumia rasilimali mbali mbali ili kuweza kufikia malengo ya pamoja. kuyafikia malengo haya watu wanatakiwa kufanya kazi kwa pamoja kwa upendo na kushirikiana. Ushirikiano huu uathiriwa na watu kujifikiria wao pekee na kutothamini mahitaji na matakwa ya wengine. Tabia ya ubinafsi hudhihirishwa na wale wasiopenda kujishughulisha na mambo ya wengine na kutokujali hisia zao huku wao wakitamani kuoneshwa kujali na kupendwa.

Mwenzao akiugua, akifiwa au kupata janga lolote ungana na wenzako kumtia moyo, akiwa na jambo la heri kama harusi na mengineyo muoneshe ushirikiano pia. Fanya yale ambayo ungependa wenzako wakufanyie pia.

UJUAJI ULIOKITHIRI

Kila mtu ana mambo anayoyafahamu na anaweza kuwa msada kwa wengine kwa namna moja ama nyingine. Wapo ambao hudhani kuwa wao wanajua kuliko wengine na hivyo wana haki ya kusikilizwa kuliko wengine. Watu hawa uwa waongeaji na kujifanya wao wanajua kila kitu na kudharau maoni na mawazo ya wengine. Hii tabia uwa ni kero kwa watu wengi na hakuna mtu anayependa kufanya kazi na watu wenye tabia hii. Jifunze kuthamini mawazo ya kila mtu na kujifunza kwa wengine. Ni vyema kuwa msikivu zaidi kuliko kuwa muongeaji.

KULETA MAMBO BINAFSI KAZINI

Umejenga nyumba, umeanza biashara mpya, au umenunua kiwanja-hongera sana, haya ni mambo mazuri na ya maendeleo lakini siyo masuala ya kupiga mbiu ofisini kila mtu ajue. Watu wanaopenda sifa ushinda wakieleza mambo yao binafsi ambayo wakati mwingine hayana tija katika kuwajenga wengine. Kwa upande mwingine wapo ambao huyaanika hata mambo yanayotakiwa kubaki kuwa siri. Umegombana na mwenzi wako au mmeachana siyo suala ambalo kila mfanyakazi anatakiwa ajue au kuyazungumza kwenye soga na wafanyakazi wenzio. Tafuta watu unaowaamini na wasiri wako wakuwaeleza mambo yako kwani usipokuwa makini utawakela wengine na kuathiri mahusino yenu kazini.

MAHUSIANO YA KIMAPENZI YA KIHOLELA

Utofauti wa kitabia hufanya wengine kudhani kuwa na wapenzi wengi au kubadilisha wapenzi mara kwa mara wakidhani ni sifa au jambo jema. Mara nyingi tabia hii usababisha maumivu kwa wengine na kuacha majeraha kwenye nafsi zao. Tabia hii husababisha kuchukiwa na watu na kufanya kuwa mfano mbaya kwa wengine. Tabia ya aina hii haivumiliki siyo maeneo ya kazi pekee bali sehemu yoyote ile. Ni vyema kujiepusha na tabia ya aina hii ili kuimarisha na kuboresha mahusinao mazuri maeneo ya kazi.

Facebook Comments

Leave a Reply

Be the First to Comment!

avatar