AINA 5 ZA MABOSI NA NAMNA YA KUENDANA NA UTENDAJI WAO KAZINI

Moja ya vitu vinavyowapa shida waajiriwa ni mabosi wao hasa pale ambapo matarajio yao hayaendani na tabia za mabosi wao. Kwa kifupi hiki ni chanzo kikubwa sana cha msongo wa mawazo maeneo ya kazi kinachosababisha wengi kushindwa kufurahia maisha yao kwenye maeneo ya kazi. Kwa upande mwingine wapo ambao wanaishi vyema na mabosi wao kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa na mabosi hao katika maeneo ya kazi. Makala haya inakueletea aina 5 za mabosi na sifa zao na jinsi ambavyo mtu anaweza kuendana nao ili kutojiongezea msongo wa mawazo zaidi unaoweza sabababishwa na migogoro kutoka kwa mabosi.

Walevi wa Madaraka

Kuweza kuimiri nafasi anayopewa mtu ya kuwaongoza wengine vyema si jambo ambalo kila mtu analiweza. Wapo ambao nafasi walizopewa zimewazidi uwezo na kujikuta wanafanya maamuzi na matendo ambayo mtu mwenye akili timamu (isiyo na kilevi cha madaraka) hawezi kuyaona kama ni ya kawaida. Mabosi wa namna hii hujawa kiburi na dharau na kuwaona wengine hasa wanaowaongoza si lolote si chochote. Wapo radhi kutoa maneno ya kuwadharirisha wengine mbele ya kadamnasi bila kujali hata umri wao. Kwa kifupi hujawa kiburi na sifa za kijinga na kudhani kuwa madaraka ya muda waliyo nayo ni ya milele.

Njia bora ya kuepuka madhara yatokanayo na maneno na matendo yao ni kufuata kanuni na taratibu huku busara ya kiwango cha juu ikitumika katika kuhusiana nao. Si vyema kujipendekeza kwa mabosi wa aina hii japo wao ni kitu wanakichopenda kwani hawana marafiki wa kudumu. Siku wakipishana na wewe wanaweza hata kuanika siri zako kwenye vikao. Kwa kifupi unatakiwa kutimiza wajibu wako na kuendelea na maisha yako.

Watafuta ukamilifu

Mara nyingi hawa hawana shida ya moja kwa moja kimahusiano ndani ya maofisi lakini shida yao moja ni kutaka kila kitu kiende kama kilivyo pangwa. Hukerwa sana na watu wasiofuata utaratibu, wasiotunza muda na wanaofanya mambo bila maandalizi ya kutosha. Mabosi hawa hutamani kila mtu afuate sheria, miongozo, kanuni na taratibu. Kila maamuzi yanapotaka kufanywa hupenda kuuliza miongozo, sheria, taratibu na kanuni zinasemaje; hawana njia ya mkato. Hakuna ubaya juu ya hili lakini kupenda ukamilifu kukizidi huchangia kupoteza muda na mambo kwenda taratibu. Wakati mwingi huchikiwa kwa sababu hawawezi kujiongeza katika maamuzi yao bila kujiridhisha na miongozo. Faida ya kuwa na mabosi wa aina hii ukweli kwamba usawa na haki hasa katika maamuzi huzingatiwa.

Ili kuhakikisha kuwa mahusinao hayaendi mlama na migogoro isiyo ya lazima haitokei ni kuhakikisha tu unafuata taratibu na kuepuka kufanya kazi kwa kulipua kwani mabosi hawa huchukulia watu wa aina hii kama wazembe na wasiofaa katika taasisi.

Walalamikaji

Hawa ni wale mabosi wenye sifa za ‘vuvuzela’. Muda wote wao ni kupiga kelele na kutafuta nani wa kumlaumu hata kwa makosa yao wenyewe. Wakikuita ofisini lazima ujiulize kwanza hivi ni kosa gani umefanya, unaweza hata kujitathmini namna ulivo vaa kabla ya kwenda kuwaona. Mara nyingi wanapenda kuwaona watu wakiwa na shughuli za kufanya kila wakati bila kujali kuwa wanahitaji kupumzika pia. Wanaweza kutumia hata nusu saa kukusema kwa kosa dogo tu; suala ambalo pengine lilihitaji  kupuuzwa tu.

Kuepuka matatizo na hawa mabosi ni vyema kutumia mbinu sawa na zile za mabosi wakamilifu lakini cha ziada ni kujitahidi kutowapa mwanya kwa kukosea pale inapowezekana. Kwa sababu hawanaga dogo ni vyema kujiridhisha kwa kila unachotaka kufanya na hata kwa kwa kuuliza wengine.

Wahamasishaji

Hawa wanaimani kuwa mafanikio ya taasisi ni matokeo ya ushawishi wao na uwezo wa fanyakazi kufanya majukumu yao ipasavyo. Hivyo hutumia muda mwingi kuwatia moyo watu na kuwakumbusha majukumu yao. Ni watu wanaopenda kujua maendeleo ya kila shughuli inayofanyanyika ili kuweka chachu ya hamasa katika kufanikisha malengo ya taasisi. Ni kama makocha wa timu ya mpira; wanajua uwezo na udhaifu wa kila mchezaji na hutumia muda mwingi sana kujenga mazingira bora yanayoweza kuongeza ufanisi kwa kila mmoja.

Hutoa maneno ya kutia moyo na hata kutoa zawadi kwa wale wanaofanya vizuri. Wakati mwingine hutumia adhabu kama njia mbadala ya kutoa hamasa ili wengine wajifunze. Kwa sababu ni watu wanaopenda kufuatilia mambo, ili kuepuka migogoro ni vyema kuwapa taarifa za maendeleo ya kazi mara kwa mara. Furaha yao ni kuona watu wanashirikiana hivyo ni vyema kujenga na kudumisha mahusiano kazini. Hawana tofauti sana na kundi la tano la mabosi.

Watu wa watu

Hawa ni wale ambao kila mtu angependa kufanya kazi nao. Wanachukulia taasisi kama familia na wanafanya jitihada kubwa kuhakikisha hakuna mwanafamilia yoyote anayekuwa na shida na isipewe uzito. Hawapendi kuona migogoro ikiendelea ndani ya taasisi  na ni watu wa kujichanganya. Milango ya ofisi zao sio migumu kuifungua na watu uwa huru kuelezea hisia, maoni na matakwa yao. Mara nyingi wako tayari kubeba uwajibika wa jumla hata kwa makosa ya wengine; yaani idara moja isipofanya vizuri wanakubali kwamba kama taasisi hatujafanya vizuri. Wako tayari kuwaendeleza wengine na kuwaandaa kushika nyadhfa mbali mbali pamoja na ile waliyonayo. Kwao mafanikio ya mtu mmoja ni mafanikio yao pia.

Kuendana na watu wa aina hii ni rahisi lakini mtu akitumia sifa zao njema kama kigezo cha kufanya anavyotaka haimaanishi kuwa watamchekea hivyo ni vyema kufurahia mazingira haya mazuri huku ukiwajibika na kujua mipaka yako. Kwa sababu siyo watu wa kuonea wengine wakifanya maamuzi magumu kama ya kukufukuza kazi bado watu watasema, “mpaka bosi amemfukuza kazi ujue kweli jamaa alikosea”. Si vyema kujisahau.

Je, bosi wako yupo kundi gani? Na wewe Je?

Facebook Comments

1 thought on “AINA 5 ZA MABOSI NA NAMNA YA KUENDANA NA UTENDAJI WAO KAZINI

  1. Pingback: AINA 5 ZA MABOSI NA NAMNA YA KUENDANA NA UTENDAJI WAO KAZINI – Kelvin Mwita

Leave a Reply

Your email address will not be published.