ULICHO KISOMA DARASANI KISIKUFUNGE KATIKA KUTENGENEZA KIPATO

Mara nyingi tunapoamua kutafuta ajira tunapenda kutathmini taaluma zetu bila kunGalia uwezo wetu. Hiki kimekuwa kikitufanya kuwa watumwa wa vyeti tulivyopata vinavyotuzuia kuona zaidi ya kile tulicho aminishwa tunaweza. Imefika hatua vijana wanasema najuta kusoma kozi fulani kwa sababu nimegundua upatikanaji wa kazi kwa kile nilichosomea ni mgumu au pengine nafasi zinazotangazwa na waajiri katika fani hiyo ni chache sana.

Baada ya kumaliza shahada ya uhasibu akili yako inakwambia kuwa unachotakiwa kufanya maisha yako yote ni uhasibu pekee na hakuna kingine.  Na kuna uwezekano kabisa kuwa uhasibu siyo wito wako lakini umejikuta katika fani hiyo bila kutarajia.  Ni vyema kuangalia ni nini waweza kifanya hata kama haukukisomea.

Katika kutafuta Ajira

Katika utafutaji wa ajira kuna haja ya kuangalia zaidi ya taaluma au fani uliyonayo. Unaweza ukawa umesomea ugavi lakini una uwezo mzuri sana wa kuwa mtoa huduma kwa wateja. Pengine unahitaji mafunzo ya muda mfupi tu au maelekezo ya nini cha kufanya na ukajikuta unaimudu vizuri kazi hiyo kuliko hata wale waliotumia miaka kadhaa kuisomea.

Ni dhahiri kuwa taasisi nyingi zinapo tangaza nafasi za ajira hutoa vigezo vinavyohitajika ili mtu anayekidhi vigezo hivyo aombe kazi. Hii imeendelea kuwa changamoto kwa sababu moja ya vigezo ambavyo uainishwa ni taaluma juu ya kazi hiyo ambayo mara nyingi hutolewa katika taasisi za elimu. Na kama hauna taaluma hiyo hicho uwa kikwazo katika mchakato mzima wa kuomba kazi hiyo.

Ukweli ni kwamba bado watu wenye nia ya kuvunja ukuta wa kitaaluma wamekuwa wakionyesha jitihada za kufanya kazi ambazo hawajasomea kabisa. Mashirika mengi hasa yale binafsi yamekuwa yakitoa mwanya kwa baadhi ya nafasi kujazwa na watu wenye sifa za kielemu zisizoendana kabisa na walichosomea darasani lakini wana uwezo wa kumudu nafasi hizo. Pia, wapo ambao wamefanya jitihada binafsi za kuamua kuomba kazi ambazo hawajazisomea kwa imani kuwa wanauwezo wa kuzifanya. Unaweza kuwa mwanasheria lakini unakipawa na wito wa kuwa mtangazaji kwa nini usijaribu fursa kwenye upande huo. Kwa hili nina amini wengi tunakubaliana kuwa wapo watangazaji ambao hawajasomea fani hii lakini ni  wazuri katika utangazaji kuliko hata wale walioisomea.

Soko la ajira katika ulimwengu wa sasa linahitaji mbinu mbadala zenye ubunifu ili kuweza kukabiliana na changamoto zake.

Ajira mbadala

Gharama za maisha zinapanda kila leo. Kwa wale walio ajiriwa watakuwa wanakubaliana na mimi kwamba mshahara haujawahi tosha kutokana na matumizi kuwa mengi. Je, kuajiriwa katika fani fulani kunatuzuia sisi kujiingiza kwenye shughuli nyingine zinazoweza kutuingizia kipato? Kuwa daktari kunazuia wewe kumiliki hata banda la kuku au biashara ya aina yoyote? Wakati mwingine usomi umekuwa kikwazo kikubwa sana cha kutuzuia kuona fursa mbali mbali zilipo katika jamii yetu. Tunadhani kuwa fani zetu pekee ndizo zinazostahili kupewa muda mwingi kwa sababu ya kile tunacho amini kuwa ujira wa uhakika.

Ni vyema kujijengea utamaduni wa kutumia uwezo na vipawa tulivyonavyo ili kujiongezea kipato. Hivi kuna chuo nchini kinachofundisha ushereheshaji (u-MC)? Lakini wapo wenye vipawa kama hivi  vinavyo waingizia mamilioni ya pesa lakini wengine wameamua kukaa navyo kisa tu kuna ujira wa uhakika kila mwezi.

Hebu tujitafakari ni nini tunachoweza kukifanya nje ya kile tunachokifanya kwa mazoea kwa sababu tu mfumo wa elimu, wazazi na jamii kwa ujumla imetuaminisha kuwa ndicho pekee tunachoweza kukifanya maishani. Fursa ni nyingi na nina amini kila mtu ana uwezo au kipawa ambacho anaweza kukitumia katika kujiongezea kipato.

Mafunzo

Katika kufanya jambo lolote jipya, uoga mara nyingi umekuwa kikwazo kikubwa sana hasa unapokuwa na wasiwasi na uwezo wako. Njia bora ya kupata uwezo ni kujiongezea ujuzi ili kumudu shughuli fulani. Ujuzi huu unaweza kupatikana katika mfumo rasmi kama vyuo, mashule na taasisi mbali mbali za mafunzo lakini pia katika mfumo usio rasmi kama kufundishwa na mtu binafsi mwenye uwezo juu ya jambo husika au kujisomea machapisho na njia nyingine kama video mtandaoni.

Katika kumudu changamoto hizi za kushindwa kufanya kitu fulani tunaweza kuamua kwenda kusomakozi fupi fupi au kuwatafuta watu wenye uzoefu na tukapata maarifa na ujuzi . Ili kuwa mkulima bora waweza jiongezea uwezo kwa kwa kujifunza kwa wakulima waliofanikiwa, vile vile kwa wafanyabiashara na wabobezi wa fani mbali mbali.

Mafunzo pia yanaweza kutumika katika kubadili fani mtu anayofanya. Wapo waliogundua kuwa wanachokifanya au walichokisomea sio wito wao na kuamua kujifunza vitu vipya ili kufanya kile ambacho wanaamini kuwa ni wito wao na kina wapa furaha zaidi na Amani kukifanya.

Usikubali kuwa mfungwa na mtumwa wa vyeti vyako. Yapo mengi unayoweza kufanya lakini haujaamua kuyafanya. Jifanyie tathmini ili ujue nini unachoweza kukifanya mbali na kile unachokifanya sasa. Ili kujua uwezo wako pia waweza uliza hata watu wako wa karibu ili wakufanyie tathmini. Unaweza jiona ni mtu wa kawaida tu kumbe una uwezo wa kufanya mambo mengi yanayoweza badili maisha yako. Usijichulie poa.

Facebook Comments

1 thought on “ULICHO KISOMA DARASANI KISIKUFUNGE KATIKA KUTENGENEZA KIPATO

  1. Pingback: ULICHO KISOMA DARASANI KISIKUFUNGE KATIKA KUTENGENEZA KIPATO – Kelvin Mwita

Leave a Reply

Your email address will not be published.